CCM yakamilisha mchakato kura ya maoni Singida Kaskazini

Muktasari:

Jimbo la Singida Kaskazini lipo wazi baada ya Lazaro Nyalandu kujivua ubunge.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, Joseph Monko ameshinda kura ya maoni CCM katika jimbo la Singida Kaskazini, baada ya kuzoa kura 21 kati ya 112 zilizopigwa.

Monko amepata ushindi katika uchaguzi uliofanyika leo Alhamisi Desemba 14, 2017 katika Kijiji cha Ilongero wilayani Singida, ukiwa ni wa marudio baada ya CCM kufuta mchakato wa awali kutokana na kuwepo tuhuma za rushwa.

Akitangaza matokeo, msimamizi wa uchaguzi huo katibu msaidizi wa idara ya oganaizesheni ya makao makuu CCM, Steven Kazindi amesema nafasi ya pili imechukuliwa na Choyo Japhet aliyepata kura 20 na mshindi wa tatu ni Manase Maghina.

Uchaguzi huo umeshirikisha wagombea 22 walijitokeza kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha ubunge jimbo la Singida Kaskazini.

Awali, uchaguzi ulifanyika Desemba 10,2017 ambao ulifutwa na vikao vya ngazi ya juu ya CCM ikilezwa uligubikwa na vitendo vya rushwa.

Kazindi amesema kura ya maoni haiteui mgombea isipokuwa inatumika kupima nani atauzika.

“Vikao vyenye mamlaka ndivyo vyenye dhamana ya kuteua mwana CCM atakayekidhi vigezo vinavyohitajika katika uchaguzi,” amesema.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuwa uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika Januari 13,2018.

Jimbo la Singida Kaskazini lipo wazi baada ya Lazaro Nyalandu kujivua ubunge alioshinda akiwa CCM na kuhamia Chadema.